| Chapter 4 |
1
| Basi, Mungu, kwa huruma yake, ametukabidhi kazi hii na hivyo hatufi moyo. |
2
| Tumeyaacha kabisa mambo yote ya aibu na ya kisirisiri. Hatuishi tena kwa udanganyifu, wala kwa kulipotosha neno la Mungu; bali tunaudhihirisha ukweli kwa kuufanya ukweli, na hivyo kujiweka chini ya uamuzi wa dhamiri za watu mbele ya Mungu. |
3
| Maana, kama Habari Njema tunayohubiri imefichika, imefichika tu kwa wale wanaopotea. |
4
| Hao hawaamini kwa sababu yule mungu wa ulimwengu huu amezitia giza akili zao wasipate kuuona wazi mwanga wa Habari Njema ya utukufu wa Kristo, ambaye ni mfano kamili wa Mungu. |
5
| Maana hatujitangazi sisi wenyewe, ila tunamhubiri Yesu Kristo aliye Bwana, sisi wenyewe tukiwa watumishi wenu kwa ajili ya Yesu. |
6
| Mungu ambaye alisema, "Mwanga na uangaze kutoka gizani," ndiye mwenye kuiangaza mioyo yetu, na kutupatia mwanga wa ujuzi wa utukufu wa Mungu uangazao katika uso wa Kristo. |
7
| Basi, sisi tulio na hazina hii tuko tu kama vyombo vya udongo, ili ionekane wazi kwamba nguvu hiyo kuu yatoka kwa Mungu wala si kwetu sisi wenyewe. |
8
| Daima twapata taabu, lakini hatugandamizwi; twapata mashaka, lakini hatukati tamaa; |
9
| twateseka, lakini hatuachwi bila msaada; na ingawa tumeangushwa chini, hatukuangamizwa. |
10
| Kila wakati tumekuwa tukichukua mwilini mwetu kifo cha Kristo, ili uhai wake Yesu pia udhihirike katika miili yetu. |
11
| Naam, katika maisha yetu yote tunakabiliwa na kifo daima kwa ajili ya Yesu, ili uzima wake Yesu udhihirike katika miili yetu inayokufa. |
12
| Hii ina maana kwamba ndani yetu kifo kinafanya kazi, lakini ndani yenu uhai unafanya kazi. |
13
| Maandiko Matakatifu yasema: "Niliamini, ndiyo maana nilinena." Nasi pia, tukiwa na moyo huohuo wa imani, tunaamini, na kwa sababu hiyo twanena. |
14
| Tunajua kwamba yule aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi pia pamoja na Yesu na kutuweka mbele yake pamoja nanyi. |
15
| Yote haya ni kwa faida yenu; ili kama vile neema ya Mungu inavyoenea kwa watu wengi zaidi na zaidi vivyo hivyo watu wengi zaidi watoe shukrani nyingi kwa utukufu wa Mungu. |
16
| Kwa sababu hiyo hatufi moyo; na hata kama maumbile yetu ya nje yataoza, lakini kwa ndani tunafanywa wapya siku kwa siku. |
17
| Taabu tunayopata ni kidogo, tena ya muda tu: lakini itatupatia utukufu upitao matazamio yote, utukufu ambao hauna mwisho. |
18
| Hivyo tunatazamia kwa makini si vitu vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Maana vinavyoonekana ni vya muda tu; lakini vile visivyoonekana ni vya milele. |